
Na Sada Amir
Muundo wa maziwa ya mama unatofautiana sana na maziwa mengine yakiwemo maziwa ya Ng’ombe na mbuzi ambayo yamekuwa yakitumiwa sana na wanawake waliojifungua kuwapa watoto wao.
Wengine uwapa watoto wao maziwa hayo kutokana na shida mbalimbali zinazowaladhimu kutonyonyesha lakini wengine huogopa kunyonyesha wakihofia kuharibu maumbile yao hivyo kuishia kuwapa watoto maziwa ya ng’ombe au mbuzi na maziwa ya kopo (yanayotokana na mimea kama vile soya au ya Ng’ombe yaliyoboreshwa).
Kwa mujibu wa Muuguzi wa Hospitali ya Aga Khan iliyopo jijini Mwanza Johari Amir anasema, kuna tofauti kubwa sana kati ya maziwa ya mama na maziwa mengine yakiwemo ya Ng’ombe na hata ya kopo.
Anasema, maziwa ya mama ni masafi, salama, yanajoto halisi, yanavirutubisho kamili na kinga zote zamwili zinapatikana kwenye maziwa ya mama tofauti na mengine.
“Maziwa ya mama huyeyushwa kwa urahisi na kufyonzwa na mwili kwa ufanisi lakini pia Huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto”anasema
Anasema, maziwa ya ng’ombe hayana vitamini E ya kutosha, madini ya chuma pamoja na asidi za mafuta muhimu inayoweza kufanya watoto wanaopewa maziwa hayo kuwa na upungufu wa chembe nyekundu za damu ambazo ni muhimu.
“Maziwa ya ng’ombe pia yana wingi wa protini, sodium na potasiamu ambayo ni vigumu kwa figo za mtoto mchanga kuondoa mabaki ya ziada ya protini mwilini yanayotokana na maziwa ya ng’ombe au mbuzi”anasema
Kutokana na hatari iliyopo kwenye maziwa ya ng’ombe anashauri kina mama wasio na shida yoyote katika unyonyeshaji wasiwape watoto maziwa ya ng’ombe au mbuzi kama chakula kwa mtoto chini ya mwaka mmoja badala yake wawanyonyeshe watoto wao bila kuwapa hata maji hadi watakapofikisha miezi sita ndio waanze kuwapa vyakula mbadala kama wanavyoshauriwa kliniki.
Anasema kwa wale wenye shida kwenye unyonyeshaji, wakamue maziwa yao kisha kuwapa watoto kwani yakikamuliwa hukaa masaa sita mpaka nane bila kuharibika au watumie maziwa ya kopo kwakuwa yameboreshwa japo hayana kinga mwili na viini vya kumkinga mtoto dhidi ya maradhi.
Afisa Lishe Mkoa wa Mwanza Sophia Lugome anasema, Virutubisho vilivyomo kwenye maziwa ya mama, wepesi na uzito wa maziwa hubadilika kutokana na umri wa mtoto na tofauti hiyo hutegemea muda mtoto anaotumia kunyonya.
Anasema, maziwa ya mwanzo uwa na rangi ya njano na hutoka siku tatu za mwanzo baada ya mama kujifungua, Baadaye maziwa ya mama huwa meupe, kutoka kwa wingi, matiti hujaa na kuwa mazito.
Anasema hakuna muda bora kati ya mchana na usiku ambao kiasi cha mafuta ni kizito kwenye maziwa ya mama bali mafuta yapo kwa asilimia tatu kwenye maziwa ya mama kwa muda wote.
“Hata maji yapo kwenye maziwa ya mama kwa asilimia 80 muda wote, ndomana tunasema chini ya miezi sita mtoto asipewe hata maji, apewe maziwa ya mama peke yake,”amesema
Anasema, Ni muhimu kumnyonyesha mtoto kwenye titi moja kwa muda wa kutosha ili aweze kupata maziwa yale ya mwisho ya kumwezesha mtoto kushiba kwakuwa uwa na mafuta mengi zaidi kuliko anapoanza kunyonya.
Ameongeza kuwa, mama anapaswa kumuacha mtoto anyonye ziwa moja kwa muda wa dakika 30 (nusu saa) kabla ya kumbadilishia ziwa lingine.
“Tunawashauri wazazi kuwa ni muhimu sana mtoto apate maziwa yanayoanza kutoka na yale ya mwishoni ili apate virutubisho vyote na maji anayohitaji”amesema