Kuna wakati huwa ni ngumu kwa wazazi kutambua nini chanzo cha kifo cha ghafla kwa mtoto mchanga, hali ambayo kwenye jamii zetu za Afrika, baadhi ya watu uhusisha hali hiyo na imani za kishirikina hasa pale inapotikea mtoto amefariki bila kuumwa akiwa usingizini.
Hii inatokana na baadhi ya wazazi kukosa elimu ya kutosha juu ya vifo vya ghafla. Takwimu zinaonesha kuwa watoto wa kiume ndio wanao athirika zaidi ya wa kike.
Kifo cha ghafla kitalamu huitwa Suddenly Infant Death Syndrome (SIDS) au (Crib Death) kinatokea kwa watoto wenye umri wa mwaka 0 hadi mmoja hutokea pindi wakiwa wamelala.
Vifo vingi huwapata zaidi watoto wenye umri wa 0 hadi miezi sita na kundi dogo la watoto wa miezi 6 hadi 12. Chanzo chake hakijajulikana moja kwa moja lakini kunavitu vinavyochochoea kwa kiasi kikubwa aina hii ya vifo.
Sababu ambazo zinaweza kusababisha mtoto wako kukumbwa na tatizo hili ni pamoja na kumlaza kwa kulalia tumbo, hii ni hatari sababu upumuaji wake unakuwa wa tabu.
Uvutaji wa sigara ndani ya nyumba au eneo alilopo mtoto ni hatari, hii ni kwa sababu mapafu yake hayajakomaa kupokea moshi mkali wenye sumu (Nicotine) hivyo, humuathiri kwa haraka zaidi.
Watoto njiti nao wako hatarini kupoteza maisha. Watoto hawa wanaozaliwa chini ya wiki 38 kwa kawaida hufariki ghafla.
Pia iwapo mama alikuwa akivuta sigara, kunywa pombe au dawa yoyote ya kulevya wakati akiwa mjamzito, anaouwezo mkubwa wa kumsababishia mtoto kifo cha ghafla.
Njia za kuepuka
Wataalamu wa masuala ya afya wanashauri kumlaza mtoto kwa kutumia mgongo na si kutumia ubavu au tumbo, kwa sababu nafasi ya kumlazia tumbo itamfanya apate hewa ya oxygen kwa kiasi kidogo na hivyo kufanya hewa ishindwe kusafirishwa kwenye ubongo ndio hapo inakuwa rahisi kwake kufariki.
Aidha, mama anaenyonyesha mtoto kwa kipindi cha mwaka na kuendelea anapunguza hatari ya kifo cha ghafla kwa mtoto kwa asilimia 50, kuliko yule anayepewa maziwa ya kopo.
Epuka kuvuta sigara ndani ya chumba alicholala au alichokaa mtoto. Sigara inaweza kumfanya mtoto asipumue vizuri. Lakini pia mnunulie ‘Pacifier’ zile chuchu za kunyonya mdomoni kwani husaidia kuzuia kifo cha ghafla.
Mtoto anapaswa kulazwa sehemu salama, utakapo mlaza kitanda cha watu wazima hakikisha asijigonge ukutani au kusiwe na mpenyo kati ya kindani na ukuta kwani anaweza kuingia kati na kukosa hewa kwa sababu ya kubanwa.
Hakikisha kitanda anacholala mtoto hakina nguo, mashuka, toys au mto kwani vitu hivi vinaweza kumziba pua na kukosa hewa hasa ukizingatia kuwa mtoto mchanga hana uwezo wa kujitoa shuka iwapo litamfunika uso.
Jitahidi kumnunulia mtoto kitanda chake kwa kuwa ni salama zaidi. Kitanda cha mtoto kinasaidia kumwepusha kujigonga kwenye ukuta au pembe za kitanda.
Epuka kumfunika na shuka kubwa au zito. Mtoto anahitaji shuka jepesi na iwapo utalala naye hakikisha humfuniki na nguo zako au shuka puani akakosa hewa au mwili ukachemka.
Ni muhimu kumwangalia mtoto mara kwa mara pindi akiwa amelala, unaweza ukamnunulia ‘baby monitor’ kwani itasaidia kumsikia akiwa anapumua, analia au anacheka inakuwa rahisi kujua kama kuna lolote linaendelea chumbani.
Usimlaze mtoto moja kwa moja baada ya kutoka kunyonya, hakikisha unamweka begani mpigepige mgongoni ili abeuwe au hata kucheuwa. Subiri badaa ya dakika 5 hadi 10 hapo ndipo unaweza kumlaza kitandani.
Ilichapishwa kwanza na Mtanzania kwenye tovuti lao https://www.google.com/amp/s/mtanzania.co.tz/unavyoweza-kumwepusha-mtoto-mchanga-na-kifo-cha-ghafla/amp/