Unyonyeshaji maziwa ya mama una faida nyingi kwa wanawake na watoto, bila kujali wanaishi nchi yenye kipato cha juu au chini au kaya tajiri na maskini.
Miongoni mwa faida za kiafya na kiuchumi za kunyonyesha maziwa ya mama ni kuweza kuokoa maisha ya maelfu ya watu na kuongeza mabilioni ya dola kwa uchumi wa dunia kila mwaka.
Jarida la Lancet katika makala zake kuhusu unyonyeshaji maziwa ya mama zinabainisha kuwa, kuongeza viwango vya unyonyeshaji duniani ni kichocheo cha msingi cha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030, kuboresha lishe, elimu na afya ya mama na kuendeleza maisha ya mama na mtoto.
Nchi nyingi zaidi zinatakiwa kuwekeza kwenye sera na mipango inayoungwa mkono maamuzi ya wanawake kunyonyesha maziwa ya mama ili kuchochea kasi ya maendeleo.
Mwakilishi mkazi nchini wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Utamaduni, Elimu na Watoto (Unicef), Maniza Zaman, anasema unyonyeshaji maziwa ya mama unaokoa maisha na kuboresha afya.
Kama hiyo haitoshi,ni njia ya kuwapa watoto lishe iliyotengenezwa kikamilifu pia ni maziwa ya mama ni dawa bora zaidi inayotibu kwa kuangalia mahitaji binafsi ya lishe ya mtoto.
Maniza anasema kuboresha unyonyeshaji kunaweza kuokoa takribani maisha ya watu 820,000 kwa mwaka, asilimia 87 kati yao wakiwa ni watoto wachanga wenye umri wa chini ya miezi sita.
“Karibu nusu ya matukio yote ya kuhara na theluthi moja ya maambukizo yote ya njia ya hewa, yanaweza kuzuilika kwa kuongeza kiwango cha kunyonyesha maziwa ya mama kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha kati,” anabainisha.
Mwakilishi huyo anabainisha kuwa ,kunyonyesha maziwa ya mama kunahusishwa na kufanya vizuri zaidi kwenye vipimo vya upeo wa kiakili kwa watoto na vijana kwa wastani wa alama tatu kwa kuzingatia mchango wa mama katika upeo wa kiakili wa mtoto.
Kwa upande wa afya za kina mama, anafahamisha kuwa upo ushahidi mkubwa zaidi kuwa, kunyonyesha maziwa ya mama kunapunguza matatizo ya unene/uzito mkubwa na kisukari baadaye maishani.
“Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa na akili zinazojitosheleza kuwa ni matokeo ya unyonyeshwaji maziwa ya mama uliokamilika unachangia kuwa na maendeleo mazuri ya kielimu, kipato na uzalishaji mkubwa katika kipindi cha muda mrefu,” anasema na kuongeza:
“Kidunia makadirio ya gharama ya upeo mdogo wa kiakili unaohusika na kutonyonyeshwa maziwa ya mama ni jumla ya takribani dola za Marekani bilioni 300 kwa mwaka.Nchi zenye kipato cha juu zinapoteza Dola bilioni 230 kwa mwaka,” anasema.
Aidha, anasema kila mwaka ambao mama ananyonyesha, uwezekano wa kupata saratani ya matiti ya hatua ya pili unapungua kwa asilimia sita na mfuko wa uzazi pia unapungua.
Mwakilishi huyo anabainisha kuwa, viwango vya sasa vya kunyonyesha maziwa ya mama tayari vinazuia vifo karibu 20,000 vinavyotokana na saratani ya matiti kila mwaka. Vifo vingine 20,000 vinaweza kuzuiliwa kwa kuboresha unyonyeshaji maziwa ya mama.
Unicef inasema, kwa Tanzania mikoa inayoonyesha mwelekeo unaotia moyo wa unyonyeshaji ni kama Kilimanjaro, Tanga na Iringa yenye asilimia 75 ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.
Pia, zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa miezi 0-5 wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi 6 ya mwanzo katika mikoa ya Iringa, Kigoma, Morogoro, Singida, Katavi na Geita, huku Kagera ikiwa na kiwango kikubwa cha zaidi ya asilimia 70.
Anabainisha kunachangia kushusha gharama za mwaka za huduma ya afya kwa jumla ya dola milioni 312 nchini Marekani, dola milioni 48 Uingereza, dola milioni sita Brazil na Dola milioni 30.3 nchini China.
Miongoni mwa changamoto zinazoanishwa katika utekelezaji ni mapungufu ya uelewa wa watoa huduma ya afya, kukosekana kwa mifumo imara ya msaada kwenye familia na jamii, pamoja na mila na tamaduni zisizounga mkono kunyonyesha maziwa ya mama.
Pia likizo fupi ya wiki sita kwa baadhi ya nchi kunaongeza uwezekano wa kutonyonyesha maziwa ya mama au kuacha kunyonyesha mapema kwa asilimia 400, kwani ni asilimia mbili ya nchi zote duniani zinakidhi mapendekezo ya Shirika la Kimataifa la Kazi ya kuweka majuma 18 kwa ajili ya likizo ya uzazi.
Mila na desturi za kifamilia na kijamii zina ushawishi mkubwa katika kuamua wanawake waungwe mkono kuhusu maamuzi yao ya kunyonyesha maziwa ya mama nyumbani, kazini na jamii kwa ujumla.
Pia, uuzwaji usiofaa wa vyakula mbadala vya maziwa ya mama unadhoofisha unyonyeshaji maziwa ya mama, kati ya mwaka 2014 na 2019 mauzo ya dunia yanatarajiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 45 hadi dola bilioni 71 ya bidhaa hizo.
“Watengenezaji na wasambazaji hutoa matangazo yanayohusiana na ulishaji wa watoto wachanga, hali inayochangia kudhoofisha unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia yenye ufanisi ya kuboresha afya katika siku za kwanza za maisha ya mtoto,” anabainisha.
Kwa upande wa Tanzania, anasema kuna kanuni ya uuzaji wa chakula mbadala na bidhaa teule ya mwaka 2013 inayolinda unyonyeshaji, lakini tatizo kubwa lipo katika ufuatiliaji na utekelezaji imara kwani wanawake wanaofanya kazi wanapaswa kusaidiwa kupitia sheria zinazolinda mifumo ya msaada ya kifamilia na jamii.
Kuhusu viwango vya kunyonyesha maziwa ya mama kuwa havijaongezeka kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita ni kwamba nchi nyingi zimeshindwa kufikia malengo yaliyowekwa kidunia. Watoto walio chini ya miezi sita wanapaswa kunyonyeshwa bila kuchanganyiwa chakula kingine lakini asilimia 37 ndiyo wanatimiza matkwa hayo, huku lengo la kidunia ni kuongeza kufikia asilimia 50.
“Pato la jumla la ndani linavyoongezeka mara mbili zaidi, unyonyeshaji maziwa ya mama kwa miezi 12 unapungua kwa asilimia 10. Chini ya asilimia 20 ya watoto kwenye nchi zenye kipato cha juu wananyonyeshwa maziwa ya mama kwa miezi 12, nchi za kipato cha chini ni asilimia 40,” anabainisha na kuongeza:
“Kunyonyesha maziwa ya mama ni njia ya asili zaidi yenye ufanisi zaidi wa gharama, iliyo rafiki zaidi kwa mazingira na rahisi zaidi tunayoijua ya kuwapa watoto wote tajiri au maskini mwanzo mzuri kiafya,”
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha chakula na lishe nchini, Dk. Joyceline Kaganda, anasema hali ya lishe Tanzania siyo ya kuridhisha kwa kuwa, tatizo la utapiamlo hususani udumavu miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka mitano limepungua kutoka asilimia 50 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2014 na iliathiri watoto takribani milioni 2.7.
“Hatua madhubuti za kuwakinga watoto dhidi ya udumavu zinafanyika katika kipindi hiki cha dhana iliyoitwa dirisha la fursa yaani kuanzia kutungwa kwa mimba, ukuaji wa mimba hadi mwisho wa miaka miwili ya uhai wa watoto,”anabainisha.
Anasema kulingana na idadi halisi zaidi ya watoto 430,000 wenye umri wa miaka mitano linapungua toka asilimia 25 mwaka 1992 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 2014, idadi ambayo inakaribia asilimia 12.5 ikiwa lengo ambalo serikali ya Tanzania imejiwekea.
“Utapiamlo umetawanyika kwa viwango tofauti baina ya mikoa na jinsia tofauti nchini Tanzania, hasa ukiwaathiri zaidi wavulana, watoto wanaoishi katika jamii zenye mapato duni na miongoni mwa watoto wanaoishi katika mikoa mahususi,” anabainisha.
Anasema taratibu muhimu za malezi ya watoto kwa ajili ya lishe bora katika maisha ya mtoto mchanga ni unyonyeshaji na ulishaji wa chakula cha nyongeza, ila tabia na taratibu za ulishaji wa watoto wachanga na watoto wenye umri mdogo bado ni hafifu.
Dk. Kaganda anasema, kiwango cha unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo miongoni mwa watoto wenye umri kati ya miezi 0-5, kiliongezeka toka asilimia 29 mwaka 1996 hadi kufikia asilika 41 mwaka 2005 na mwaka 2014 asilimia 42.
Upande wa visiwani ni asilimia 20 ya watoto wenye umri wa chini ya miezi sita wananyonyeshwa bila kuchanganya maziwa ya mama na vitu vingine, asilimia 51 ya watoto Tanzania Bara na asilimia 62 wananyonyeshwa katika kipindi cha saa ya kwanza baada ya kuzaliwa.
Kuhusu ulishaji watoto vyakula vya nyongeza, asilimia 25 ya watoto wenye umri wa kati ya miezi 6-23 wanapata chakula cha mchanganyiko wa vyakula mbalimbali kwa Tanzania Bara dhidi ya asilimia 12 Visiwani Zanzibar, huku asilimia 20 ya watoto Tanzania Bara wanapata milo yenye mchanganyiko wa vyakula mbalimbali na kulishwa idadi ya milo inayokubaoika dhidi ya asilimia nane visiwani.
Anasema idadi ya watoto kitaifa wanaopata wastani wa milo inayopendekezwa kwa siku ni asilimia 66 kwa Tanzania Bara na asilimia 54 visiwani.
Mkurugenzi huyo anasema, upungufu wa damu miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ulipungua toka asilimia 72 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 59 mwaka 2010, huku theluthi moja ya watoto wanaathirika na upungufu wa vitamini asilimia 33, kwani ni asilimia 8.3 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wenye watoto chini ya miaka mitano waliwahi kutumia vidonge vya madini ya chuma na asidi ya foliki.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Neema Joshua, anasema watu wengi hawana uelewa kwamba mtoto anapaswa kunyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa na baadhi ya wahudumu wa afya wanashindwa kuwaelekeza mama waliojifungua.
“Ukifuatilia katika hospitali zetu, Vituo vya Afya na Zahanati watoto wengi hawanyonyeshwi ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa au kupewa maziwa ya mama bila kuchanganyiwa na chochote ndani ya miezi sita na baadhi ya watumishi wa afya hawawaelezi akina mama jambo ambalo ni lazima hatua zichukuliwe katika kujenga kizazi kizuri kijacho.
Source: Nipashe