Na Flora Wingia na Mtandao
Wanawake wengi wamekuwa wakipata shida sana pale watoto wao wanapokosa hamu ya kula chakula. Ni tatizo la kawaida lakini huwapa wazazi hawa hofu juu ya afya za watoto wao.
Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha kukosa hamu ya chakula na pale inapotokea mama anapaswa kuwa mtulivu na makini katika kuchunguza nini kinaweza kuwa chanzo cha mtoto kukosa hamu ya kula. Hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya, lazima kuwapo chanzo chake.
Zipo sababu zinazoweza kutatuliwa na mzazi, lakini zingine zinaweza kusababishwa na magonjwa, hivyo ni muhimu utafutwe msaada wa wataalamu wa afya.
Magonjwa ni moja ya sababu kubwa inayowakosesha watoto hamu ya kula. Kwa mfano, magonjwa ya malaria, kuharisha, maumivu ya tumbo, maumivu ya kichwa, magonjwa ya kinywa na koo, homa na mafua au dalili nyinginezo ambazo humkosesha mtoto raha na kushindwa kula chakula.
Matatizo ya kifamilia na msongo, ni sababu nyingine ambayo huwakosesha watoto raha na hamu ya kula. Kama walivyo watu wazima. Watoto pia hukumbana na matatizo ya kifamilia kama kupoteza ndugu au vitu wavipendavyo.
Pia, watoto hukumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha kama vile majukumu ya shule au pengine unyanyasaji dhidi ya nafsi yake, kama vile kuzomewa na mambo mengine mengi yanayokiuka haki zao.
Kwa hiyo, ili kumuepusha mtoto na ukosefu wa hamu ya kula, wazazi na walezi wanapaswa kuwa, makini endapo wataona kuna mabadiliko yoyote ya kitabia ya mtoto.
Kugundua na kuziondoa sababu zinazomletea mtoto msongo, tutaweza kuwarudisha katika hali ya kawaida na hamu ya kula itarejea tena.
Aidha, wakati mwingine hali hiyo hutokana na ugonjwa wa kukosa hamu ya kula ujulikanao kitaalamu kama Anorexia nervosa. Watoto wenye ugonjwa huo, wanaweza kukaa kwa muda mrefu bila ya kula, ingawa hawana tatizo jingine na endapo watapewa chakula, huchagua aina fulani tu ya vyakula.
Ni hali inayomnyima mlo ulio kamili na kumfanya apungue uzito, kisha anadhoofika kiafya. Jambo hilo linapojitokeza, ni vyema kumpeleka mtoto kwa wataalam wa afya wa masuala ya lishe ambao watakuwa msaada mkubwa katika kumsaidia mtoto wako kurejesha tena hamu ya kula.
Kiwango kidogo cha ukuaji mtoto, huchangia kupungua kwa hamu ya kula. Katika mwaka wa kwanza wa maisha ya watoto, huwa wanakua haraka, lakini baada ya mwaka mmoja, kiwango cha ukuaji hupungua na kiwango cha chakula wanachokula pia hupungua. Katika wakati huo, hali hiyo ni ya kawaida katika maisha ya watoto.
Dawa, Minyoo na Anaemia
Sababu nyingine zinazochangia watoto kukosa hamu ya kula, ni kama vile hali ya kutopenda dawa, upungufu wa damu, kuwa na minyoo tumbon na matatizo ya mengine kama vile anaposhindwa kupata choo.
Maudhi ya dawa mbalimbali ambazo hutumika kutibu magonjwa kwa watoto, yanaweza kuchangia watoto kukosa hamu ya kula. Mfano, daktari akimwandikia mtoto dawa aina ya antibaiotiki, zinaweza kusababisha tazizo la kukosa hamu ya kula.
Kupoteza hamu ya kula kwa watoto wanaotumia antibaiotiki, kuna wakati inatokana na kujihisi maudhi dhidi ya dawa wanayopatiwa watoto wengi. Dawa nyingine, zinasababisha kichefuchefu na kutapika. Tatizo hilo humalizika, pale mtoto anapomaliza dawa na kupona.
Uambukizi wa minyoo unachangia tatizo hilo. Minyoo huingia katika mfumo wa mmeng’enyo wa watoto na kusababisha upotevu wa damu. Minyoo hutegemea ufyonzaji wa damu kama chakula chao na katika uambukizi sugu, inamfanya mtoto huyo kuvuja kwa damu, kuwa na upungufu wa damu, kuharisha, kichefuchefu, anatapika na kukosa hamu ya kula.
Endapo mtoto ataonyesha dalili za uambukizi wa minyoo, ni vyema kuwaona wataalam wa afya, ili afanyiwe vipimo na kupatiwa matibabu.
Ugonjwa wa upungufu wa damu ambao kwa kitaalam hujulikana kama anemia, husababishwa kwa watoto na tatizo hilo. halio ya kuwa na kiwango kidogo cha madini ya chuma katika damu, inawapata watoto ambao hawapati lishe ya kutosha yenye madini hayo.
Pia, anemia inaweza kusababishwa na uambukizi wa minyoo au hata magonjwa mengine. Watoto wenye anemia huwa wadhaifu na wasio wachangamfu, na kama ugonjwa usipotibiwa haraka, inaathiri afya ya mtoto na hata maendeleo yake shuleni. Ni vyema mtoto akafanyiwa vipimo vya damu, endapo itahisiwa au ataonyesha dalili za anemia.
Kwa watoto hasa wadogo, kukosa choo hupelekea kukosa hamu ya kula. Kwa hiyo inapotokea hivyo, ni vyema wakapata msaada wa wataalam, ili waondokane na tatizo hilo.
Amgalizo kwa wazazi
Wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia yafuatayo, ili kuboresha hamu ya kula na lishe kwa watoto wao:
Kuwa na ratiba nzuri ya kumpa mtoto chakula na mtoto apewe chakula anapokuwa na njaa.
Usiwagombeze au kutoa maonyo makali kwa watoto wakati wa kula.
Mpe mtoto kiasi kidogo cha chakula lakini mara nyingi kwa siku na siyo kumshindilia kwa wakati mmoja.
Usimlazimishe mtoto kula kama hana njaa.
Hakikisha mtoto anashiriki katika michezo, kwa kuwa michezo huusisha matumizi ya nishati ya mwili na kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.
Wakati mwingine mpe nafasi mtoto wa uchaguzi wa chakula akipendacho, lakini chini ya uangalilizi wa mzazi au mlezi ili afanye uchaguzi ulio sahihi.
Wakati wote wazazi na walezi wakumbuke kuwa tatizo la kukosa hamu ya kula, ni la kawaida kwa watoto wengi na tatizo linapojitokeza, hawahitajiki kuwa na wasiwasi kila wakati.
Kama mtoto wako ana afya njema, anapata usingizi vizuri na ni mwenye furaha, hakuna sababu ya mzazi kuwa na wasiwasi, lakini kama tatizo litaendelea kwa muda mrefu, basi mzazi hana budi kuonana na wataalam wa afya kwa msaada zaidi.
Source: Hii makala ilichapiswa kwanza na Nipashe
Source: https://www.ippmedia.com/sw/makala/zijue-sababu-zinazokosesha-watoto-hamu-ya-kula