Na Christina Mwakangale
*Mama ukijifungua ndani ya saa moja uwe umenyonyesha
*Mgusishe mtoto chuchu hata kama hazitoi maziwa
MARA nyingi kinamama wakijifungua familia au jamii huamini kuwa ili maziwa yatoke ni
lazima kula vyakula vya aina fulani, akiwa ni pamoja na uji wenye pilipili mtama na
mbegu za mafuta kama alizeti.
Yote hayo, wataalamu wanasema hayasababishi mama aliyejifungua kuanza kutoa
maziwa kwa vile uzalishaji na utoaji maziwa ni kazi inayofanywa na ubongo na hisia hivyo
si lazima kula pilipili manga.
Dk. Sifa Eli, kutoka Hospitali ya Magomeni jijini Dar es Salaam, akizungumza na Nipashe
kuhusu maziwa na unyonyeshaji watoto wachanga anasema ni lazima ufanyike ndani ya
saa moja baada ya kujifungua na mama ahakikishe kuwa amemnyonyesha mtoto.
“Mtoto anapozaliwa baada ya saa moja anyonyeshwe hata kama maziwa ya mama
hayatoki.”
Anaonya kuhusu dhana au fikra potofu kwa baadhi ya kinamama kwamba, anapotoka
kujifungua maziwa yanakuwa hayajaanza kujitengeneza na kutoka.
Anasema, msongo, furaha kupitiliza hupoteza maziwa na iwapo mama aliyejifungua
akipata msongo wa mawazo au furaha iliyopitiliza anaweza kusababisha uzalishaji wa
maziwa kutofanyika ipasavyo na kwa wakati.
“Kinachofanya maziwa yaanze kutoka ni ubongo, hisia, baadhi wanadhani hadi mama ale
vyakula vya aina fulani, au uji wa pilipili manga si lazima. Cha msingi, awe huru kifikra
bila msongo,” anasema Dk. Sifa.
Anataja baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha maziwa yasitoke kuwa ni pamoja na
mama kuwaza kupindukia mathalani, wapi atapata pesa ya kula, matunzo ya mwanawe na
matokeo yake ni kuzuia maziwa kujitengeneza.
Anasema pia maziwa ya mama yanaweza yasitoke kutokana na baadhi ya kinamama
kutumia dawa za tiba mbalimbali, bila kufuata ushauri wa kitabibu na kuwakumbusha
kuwa kama unayenyonyesha usinunue dawa na kumeza ila cha muhimu ni kufika
hospitalini au kituo cha afya na daktari atafahamu dawa gani atampatia kwa kuwa
ananyonyesha.
“Mtoto agusishwe chuchu saa moja ya kwanza,” Dk. Sifa anafafanua na kuongeza kwamba
zipo sababu ambazo zinaweza kusababisha maziwa ya mama aliyetoka kujifungua
yasitoke, akitaja msongo wa mawazo au kuwa na furaha kupindukia baada ya kumuona
mwanawe kuchangia.
Anaainisha kwamba, mama ambaye hajajiandaa kunyonyesha, anaweza kusababisha
maziwa yasitoke sababu yanaanza kutokana na hisia baada ya taarifa kupelekwa
ubongoni, kuwa mtoto amezaliwa.
Kadhalika anasema saa ya kwanza ya mwanzo mtoto atakapozaliwa apelekwe kwenye
ziwa chuchu ili aanze kunyonya, aiguse hata kama hayajaanza kutoka. Hatua hii itapeleka
ujumbe moja kwa moja kwenye ubongo kwamba mtoto amezaliwa hivyo maziwa
yatengenezwe.
Sifa anaongeza kuwa, mama akichelewa kunyonyesha maziwa yatachelewa pia kuanza
kutoka na kuwataka kinamama waliotoka kujifungua kuwaweke watoto wao kwenye
chuchu mara kwa mara ili ujumbe uende mara nyingi ubongoni maziwa yatengenezwe,
3/4
ndani ya nusu saa yanategemewa kuwa yanatengenezwa.
MZAZI USILALE FOFOFO
Aidha, Sifa anasema wakati wa usiku mama anayenyonyesha hatakiwi kulala usingizi
muda mrefu au kwa saa nyingi, kwa kuwa itasababisha uzalishaji wa maziwa kupungua.
“Kulala fofofo, yaani mama anasema usiku na mwanangu tumelala usingizi mzito hadi
asubuhi hii sawa. Mama unayenyonyesha asilale usiku kucha, nyonyesha kila mara, usiku
na mchana,” anahimiza Dk. Sifa.
Anawataka waliojifungua kwa njia ya upasuaji kunyonyesha watoto wao katika muda wa
saa moja.
“Kikubwa ni mama kujiamini hata kama umefanyiwa upasuaji utasaidiwa na wahudumu
wa afya ili uendelee kunyonyesha, saa ya kwanza ni muhimu sana kwa maendeleo na
mchakato wote wa ukuaji.”
SAA MOJA UKIJIFUNGUA
Dk. Sifa anahimiza kumnyonyesha mtoto saa moja baada ya kuzaliwa kuwa ni lazima kwa
michakato ya ukuaji na ni hatua muhimu ya mwanzo ya kujenga kinga imara katika
mustakabali wa kukua kwa watoto.
Katika ngazi za kimataifa, kutokana na umuhimu wa kunyonyesha Umoja wa Mataifa
(UN) uliitangaza wiki maalumu ya unyonyeshaji duniani inayofanyika kuanzia Agosti
Mosi kila mwaka, kutoa msisitizo kwa jamii kuunga mkono kuwanyonyesha watoto
wachanga kwa afya ya mataifa na dunia kote ili kuwa na watu wenye afya.
Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) pamoja na
Shirika la Afya Duniani (WHO) linatathmini kuwa, ongezeko la kiwango cha unyonyeshaji
wa maziwa ya mama pekee, linaweza kuokoa maisha ya watoto 820,000 kila mwaka.
MAZIWA NI LISHE
Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Shirika la Chakula na Lishe (TFNC), Sikitu Kihinga,
anasema katika Siku ya Unyonyeshaji Duniani mwaka huu, anakumbusha kuwa miezi sita
ya kumlisha mtotto maziwabila kumpa chakula kingine ni kuimarisha kinga dhidi ya
magonjwa na kukuza afya ya akili.
Anaungwa mkono na Ofisa Mtafiti Mwandamizi wa shirika hilo, Gelagister Gwarasa,
anayeeleza kuwa madhara ya kumlisha vyakula vingine badala ya maziwa mtoto wa chini
ya miezi sita,ni utapiamlo, mzio au aleji, kuhara na kupunguza uhusiano kati ya mama na
mtoto.
Katika hilo, Ofisa Lishe wa UNICEF-Tanzania, Tuzie Edwin, anasema kukosa muda wa
kunyonyesha watoto ni changamoto inayowakabili wazazi wanaofanya kazi na kuwataka
waajiri kuweka mazingira hata ikibidi kuwajengea eneo kwa ajili ya kinamama
kunyonyesha.
4/4
“UNICEF tuna chumba maalum kwa ajili ya kinamama kunyonyesha watoto wao, lakini
kukamua maziwa. Tumezingatia mazingira ambayo ni rafiki kwa mama na mtoto
pia.Tunaiasa jamii, familia na serikali kuhamasiha mazingira rafiki kwenye sehemu za
kazi, ili kufanikisha kumnyonyesha motto miezi sita.”
FAIDA ZA KUNYONYESHA
Umoja wa Mataifa, unazitaja kuwa ni pamoja na kuleta afya, kinga imara, kuimarisha
hisia kati ya watoto na kinamama lakini huweka mfumo endelevu wa chakula kwa watoto.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tedros
Ghebreyesus, katika siku ya unyonyeshaji anasema kinamama wanahitaji msaada ili
kuanza na kuendelea kunyonyesha.
“Wakati unyonyeshaji ni mchakato wa asili, lakini sio rahisi wakati wote,” anasema
Ghebreyesus.
Pia anatoa wito kwa serikali kulinda na kuongeza fursa za kupata ushauri nasaha kuhusu
unyonyeshaji.
Source: Ilichapishwa na Nipashe