Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana kwa sababu humpatia mama virutubishi muhimu kulingana na hali yake. Wakati wa ujauzito mama anahitaji virutubishi zaidi kwa ajili ya maendeleo yake kiafya pamoja na mtoto aliyetumboni. Lishe bora huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto kukuwa vizuri kimwili na kiakili.
Ukosefu wa lishe bora wakati wa ujauzito huweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile: mama kutoongezeka uzito kama inavyotakiwa na hivyo kukosa nguvu, upungufu wa damu wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ambao huweza kusababisha hata kifo, uwezekano wa mimba kuharibika, mtoto kufia tumboni, kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu, kuzaa mtoto njiti au kuzaa mtoto mfu na kuongezeka kwa magonjwa kwa sababu ya mfumo wa kinga kuwa dhaifu.
Matatizo haya yanazuilika kwa kuzingatia kanuni za lishe bora kwa mama mjamzito katika kipindi chote cha ujauzito.
Mambo ya kuzingatia
Ili kuhakikisha lishe bora kwa mama mjamzito inashauriwa kufanya mambo yafuatayo:
Kula milo minne kwa siku na asusa au vitafunwa mara nyingi kadri uwezavyo hii itakuwezesha kuupa mwili nguvu na lishe ya kutosha kwa ajili yako na mtoto anayekua tumboni. Hakikisha mlo wako unakuwa na vyakula mchanganyiko vinavyopatikana katika jamii. Asusa au vitafunwa vinaweza kuwa vitu kama vile mahindi ya kuchoma au kuchemsha, kikombe cha maziwa, viazi, mayai, karanga, matunda n.k.
Kuepuka kunywa kahawa au chai wakati wa mlo kwani huingiliana na ufyonzwaji wa virutubisho katika mwili.
Kumeza vidonge vya kuongeza damu (FEFO) kila siku kwa kipindi chote cha ujauzito.
Kuongeza ulaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama mfano nyama, kuku, samaki, dagaa n.k. Vyakula vya asili ya wanyama huongeza damu kwa haraka zaidi.
Kula matunda ya aina mbali mbali yanayopatikana kwa msimu huo na mbogamboga kwa wingi kila siku
Kula vyakula vilivyoongezwa virutubishi, kwa mfano unga wa ngano, unga wa mahindi na mafuta ya kupikia.
Kutumia chumvi yenye madini joto wakati wote
Kunywa maji ya kutosha kila siku (angalau glasi 8 au lita 1.5). unaweza ukaongeza ladha kwa kuweka limau au ndimu.
Kujikinga na Malaria kwa kutumia vyandarua vilivyowekwa viwatilifu na kutumia dawa za kuzuia malaria na minyoo kama inavyoshauriwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya ngono na virusi vya UKIMWI
Kuepuka utumiaji wa sigara na pombe kwani inaathiri matumizi ya virutubishi na afya ya mama na mtoto.
Kuanza kliniki mapema mara tu ya kujihisi mjamzito na uendelee kuhudhuria ili kupata huduma na ushauri zaidi utakaoboresha lishe na afya kwa ujumla.
Source: Imechapishwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania
Link: https://www.tfnc.go.tz/tips/lishe-ya-mama-mjamzito