Wakati wiki ya unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama ilianza rasmi Agosti Mosi, dunia ilahimizwa kuepuka kampeni zinazoendeshwa na baadhi ya wazalishaji wa vyakula vya watoto kuwa, kunyonyesha kunaweza kusambaza COVID-19 kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kwamba bidhaa zao ndio salama, na badala yake wananchi wanatakiwa kuhakikisha unyonyeshaji unaendelea kwani ni salama.
Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la afya Ulimwenguni, WHO na la kuhudumia watoto UNICEF katika taarifa yao ya pamoja wamehimiza makampuni kuzingatia sheria za kutafuta masoko, watoa huduma za afya kwa mama na mtoto kuhakikisha wana taarifa sahihi na vifaa vya kuweza kuwaelimisha jamii, na waajiri wa makampuni wamekumbushwa kutenga maeneo rasmi ya kunyonyesha na kuwaruhusu wakina mama kuwa na muda wakunyonyesha watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amesema unyonyeshaji ni msingi wa kujitolea. “Kuanza kunyonyesha ndani ya saa ya kwanza ya kuzaliwa, ikifuatiwa na unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa miezi sita na kuendelea kunyonyesha hadi miaka miwili au zaidi hutoa safu kali ya ulinzi dhidi ya aina zote za utapiamlo wa watoto, pamoja na kuondoa kunenepa kupita kiasi. Kunyonyesha pia ni kama chanjo ya kwanza ya watoto, kuwalinda dhidi ya magonjwa mengi ya kawaida ya utotoni.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus katika ujumbe wake wa wiki ya unyonyeshaji amesema wakati kumekuwa na maendeleo katika viwango vya unyonyeshaji katika miongo minne iliyopita, na ongezeko la asilimia 50 katika kuenea kwa unyonyeshaji wa kipekee ulimwenguni, janga la Corona linaweza kuleta udhaifu.
“Katika nchi nyingi, janga hilo limesababisha usumbufu mkubwa katika huduma za msaada wa kunyonyesha, huku likiongeza hatari ya ukosefu wa chakula na utapiamlo. Nchi kadhaa zimeripoti kuwa wazalishaji wa vyakula vya watoto wameongeza hatari hizi kwa kutumia hofu isiyo na msingi kwamba kunyonyesha kunaweza kusambaza COVID-19 na kutangaza bidhaa zao kama njia mbadala salama ya kunyonyesha” amesema mkuu huyo wa WHO.
Kauli mbiu ya mwaka huu ya wiki ya unyonyeshaji ni “Kinga unyonyeshaji: Jukumu la pamoja”.
Mwanzoni mwa mwaka huu 2021, serikali wahisani, asasi za kiraia pamoja na sekta binafsi ziliungana katika uzinduzi wa lishe ya mwaka wa utekelezaji wa lishe, ikiwa ni fursa ya kihistoria ya kubadilisha njia ya kuondoa utapiamloa kwa watoto
Mwongozo wa UNICEF
Katika hatua nyingine UNICEF imetoa mwongozo wa unyonyeshaji katika kipindi cha janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Mwongozo huo umeeleza mambo kadhaa ikiwemo, mama anayenyonyesha anaruhusiwa kupata chanjo ya COVID-19, na iwapo anahisi kuumwa anaruhusiwa kuendelea kumnyonyesha mtoto kwa kutumia kikombe kisafi, na anatakiwa kuzingatia miongozo yote ya usafi ikiwemo kunawa mikono.
Pia mwongozo huo umetanabaisha hakuna taarifa yeyote iliyoonesha mtoto ameambukizwa Corona kutoka kwa mama anayenyonyesha hivyo hata mama akibainika amepata Corona anatakiwa kuendelea kunyonyesha mtoto.
Source: UNICEF
Link: https://news.un.org/sw/story/2021/08/1124452